Rais William Ruto amepongeza timu ya taifa ya soka ya kina dada Harambee Starlets kwa ushindi katika msururu wa michuano ya FIFA ambao ni wa kwanza kabisa kwa timu za wanawake.
“Pongezi Harambee Starlets kwa ushindi wenu wa ajabu dhidi ya India, uliowahakikishia nafasi katika fainali za msururu wa FIFA wa wanawake,” aliandika Rais William Ruto.
Aliendelea kusema kwamba timu hiyo imefanya wakenya wawe na cha kujivunia huku akiihakikishia kwamba, “Mnapoingia kwenye fainali, fahamu kwamba Taifa zima linasimama na nyinyi.”
Timu ya Harambee Starlets iliishinda timu ya India mabao mawili kwa sufuri katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo jana Jumamosi jioni.
Dakika mbili tu baada ya mchuano wa jana kuanza, Martha Amunyolete alitia kimiani bao la kwanza katika kile kilichoonekana kama kutumia fursa ya kucheza mbele ya mashabiki wa nyumbani.
Kina dada hao wanaofunzwa na Beldine Odemba sasa wanatarajiwa kuchuana na Australia katika fainali ya msururu huo wa kina dada wa FIFA Jumatano Aprli 15, 2026.
Australia wanachukuliwa kuwa timu kali ikitizamiwa kwamba waliishinda Malawi mabao matano kwa nunge lakini Harambee Starlets pia wana imani ya kuibuka na ushindi kwenye fainali hiyo.