Moto wateketeza ghala la pombe Uthiru, Nairobi

Moto huo wa alfajiri ulizuka katika ghala la pombe ndani ya makazi ya Ushirika huko Uthiru.

Marion Bosire
1 Min Read

Mali ya thamani isiyojulikana imeharibiwa asubuhi ya leo Jumapili, Aprili 12, baada ya moto kuzuka ndani ya mtaa wa makazi huko Uthiru, kaunti ya Nairobi.

Moto huo wa alfajiri ulizuka katika ghala la pombe ndani ya makazi ya Ushirika huko Uthiru, na kuwashtua wakazi bila kutarajia.

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi mkubwa ukitoka ndani ya ghala hilo, huku wakazi wa eneo hilo wakijitahidi kuuzima kwani ulitishia kusambaa hadi majengo ya jirani.

Maafisa wa huduma za zimamoto walifika katika eneo la tukio huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana, ingawa hakuna majeruhi kutokana na tukio hilo.

Walioshuhudia kisa hicho, walisema moto ulizuka saa kumi na moja alfajiri, ukiwashitua waliokuwa wakiburudika usiku kucha pamoja na wakazi walioamka mapema.

Inaripotiwa kuwa moto huo ulienea haraka baada ya kuanzia katika sehemu ya ghala la pombe kali, ambazo hushika moto kwa urahisi na zinaweza kuongeza kasi ya kusambaa kwa moto katika hali kama hiyo.

Tukio hili la karibuni linaongeza wasiwasi kufuatia ongezeko la visa vya moto katika maeneo ya makazi ya Nairobi, ambayo kwa bahati mbaya mara nyingi hutokea alfajiri au nyakati za jioni.

Share This Article