Rais William Ruto ameongoza maadhimisho ya miaka 16 tangu kurasimishwa kwa Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Hafla hiyo iliyoandaliwa katika Ukumbi wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) jijini Nairobi ilihudhuriwa na viongozi wakuu serikalini miongoni mwa viongozi wengine.
Akiongoza sherehe za Katiba Dei, Ruto alitoa changamoto kwa viongozi wote kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha utekelezaji kamili wa katiba hiyo kwa vitendo na wala siyo tu nadharia.
Rais alitaja hatua zilizopigwa na utawala wake wa miaka minne, ikiwemo uboreshaji na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa Wakenya wote, jinsi ilivyoainishwa kwenye katiba kipengee cha 43, ikiwa mojawapo wa haki za kimsingi kwa kila Mkenya.
Alifafanua kuwa serikali yake imeafikia maendeleo makubwa katika sekta ya afya ambapo zaidi ya Wakenya milioni 32.4 wamesajiliwa katika bima ya SHA na wengine zaidi ya milioni 8 kupokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya kote nchini.
Aidha, aliongezea kuwa kufikia leo, wahudumu wa afya ya jamii zaidi ya laki moja wameajiriwa na kutoa huduma kwa familia zipatazo 922.
Ruto pia alitaja ufanisi mkubwa wa serikali yake katika sekta ya ujenzi na nyumba ambapo nyumba 274,000 za gharama nafuu zimejengwa na kubuni nafasi za ajira zaidi ya milioni 1.1.
Katika sekta ya elimu chini ya Katiba ya mwaka 2010, Rais alisema serikali yake imewaajiri walimu zaidi ya laki moja na kujenga madarasa 23,000, hivyo basi kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto.
Rais aidha, alisikitishwa na maandamano ya vijana kupinga serikali huku wengine wakiuawa akisema maandamano ni haki ya kila mmoja kulingana na katiba na vijana hao sawa na Mkenya yeyote, walipaswa kulindwa.
Hata hivyo, aliwakashifu wavunjaji sheria wanaochukulia fursa ya maandamano ya amani kupora na kuharibu mali.