Sasa ni rasmi kuwa Douglas Kanja Kirocho ndiye Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) mpya.
Hii ni baada ya Kanja kuteuliwa na Rais William Ruto kujaza wadhifa huo, saa chache baada ya uteuzi wake kuidhinishwa na bunge jana Jumatano.
“Kwa kutumia mamlaka niliyopewa na Kifungu Nambari 245 (2) (a) cha Katiba ya Kenya, Mimi, William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi, namteua – Douglas Kanja Kirocho kuwa Inspekta Jenerali wa Huduma ya Taifa ya Polisi kwa kipindi cha miaka minne,” kiongozi wa nchi alisema kupitia gazeti rasmi la serikali lililochapishwa jana Jumatano.
Kabla ya Kanja kuteuliwa kwenye wadhifa huo, Gilbert Masengeli amekuwa akihudumu kama kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi.
Hata hivyo, Masengeli amekumbana na changamoto za kila nui kiasi kwamba mahakama imemhukumu kifungo cha miezi 6 jela kwa kuidharau.
Masengeli ana hadi hii leo Alhamisi kutii agizo la mahakama na kufika mbele yake kuelezea waliko wanaharakati watatu wanaodaiwa kutekwa nyara na polisi mwezi mmoja uliopita la sivyo aanze kutumikia kifungo hicho.
Duru zinasema Masengeli huenda akaazimia kufika mbele ya Jaji Lawrence Mugambi baadaye hii leo ili kukwepa makali ya kifungo hicho.
Wadhifa wa Inspekta Jenerali wa Polisi ulisalia wazi kufuatia kujiuzlu kwa Japhet Koome mwezi Julai mwaka huu.
