Ruto airai jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kudumisha amani Haiti

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto akiwa na Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille katika Ikulu ya Nairobi
Rais William Ruto ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kurejesha amani nchini Haiti. 

Kenya imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi hizo na tayari imetuma maafisa 400 wa polisi kama sehemu ya kikosi cha kimataifa cha kudumisha amani nchini Haiti.

Taifa hilo la Carribean linakumbana na changamoto za kiusalama ambazo hususan zimesababishwa na magenge ya wahalifu.

“Ili kuhakikisha amani, uthabiti na usalama wa Haiti, washirika wetu wa kimaendeleo lazima waharakishe kutoa michango yao kwa maafisa wa usalama, mipango ya usafirishaji na fedha za kudumisha na kupanua kikosi hicho,” alisema Rais Ruto ambaye ameahidi kutuma maafisa zaidi wa polisi nchini humo kufikia mwezi Januari mwakani.

Ruto amesema Kenya ina rasilimali zinazotosha kukidhi mahitaji ya maafisa wake nchini Haiti hadi kufikia mwisho wa mwezi Machi mwaka ujao.

Aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa pamoja wa wanahabari akiwa ameandamana na Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa.

Conille, aliyewasili nchini Kenya jana Alhamisi, anafanya ziara rasmi ya siku nne nchini humo.

Share This Article