Rais William Ruto amezindua miradi kadhaa ya maendeleo katika kaunti ya Kajiado siku ya Jumatatu, alipoendeleza ziara yake ya kukutana na wananchi.
Baadhi ya miradi hiyo ni uzinduzi wa barabara ya Kahara-Ngong katika eneo bunge la Kajiado Kaskazini, inayogharimu serikali shilingi milioni 100.
Aidha, Rais pia alizindua barabara ya uwanja wa michezo wa Ngong inayolenga kuimarisha biashara katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto alitoa wito kwa Wakenya kukatalia mbali ukabila na siasa za migawanyiko.
“Sharti tukatae ukabila na aina zote za siasa za migawanyiko ambazo zinaathiri ajenda yetu ya maendeleo ya taifa,” alisema kiongozi wa nchi.
“Tutaendelea kufanya kazi kuelekea Kenya moja ambako kila mwananchi na kila jamii ana fursa sawa ya kunufaika kutokana na maendeleo ya taifa letu.”