Riadha ya Olimpiki ndani ya uwanja kuanza rasmi Ijumaa

Dismas Otuke
2 Min Read

Mashindano ya riadha ndani ya uwanja katika makala ya mwaka huu ya michezo ya Olimpiki yataanza rasmi Ijumaa Agosti 2, katika uwanja wa Stade de France jijini Paris,Ufaransa  miaka mitatu tangu mashindano ya Tokyo. 

Kutakuwa na jumla ya mashindano 48 yakiwa 23 ya wanaume na mengine 23 ya wanawake ,mashindano mawili ya mseto mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti  na kilomita 35 matembezi kwa jinsia mseto .

Maeneo matatu yatatumika kwa riadha ikiwemo nje ya hoteli ya de Ville na Les Invalides ambapo mbio za marathon na matembezi zitaanzia  mtawalia na pia uwanja wa Stade de France.

Kenya,inayowashirikisha wanariadha 53 inashiriki katika mashindano ya: mita 100,400,400 kuruka viunzi kwa wanaume na pia mita 800,1500,3,000 kuruka viunzi na maji, 5,000,10,000 na marathon kwa wanaume na wanawake.

Kenya pia inashiriki shindano la mita 400 kwa wanariadha wanne mseto kupokezana kijiti, na Urushaji sagai likiwa shindano pekee la ndani ya uwanja.

Katika siku ya kwanza Ijumaa, Kenya itashiriki mbio za mita 1,500 mchujo wanaume ,mita 5,000 wanawake mchujo, mita 400 kupokezana kijiti mseto ,mita 800 mchujo wanawake na mita 10,000 wanaume fainali.

Kenya ilinyakua dhahabu mbili za uwanjani miaka mitatu iliyopita katika mbio za mita 1500 wanawake na 800 wanaume na pia marathon ya wanaume na wanawake.

Kinyume na makala ya awali ya Olimpiki washindi wa dhahabu mwaka huu katika  fani 48 za riadha ,watatuzwa dola 50,000 takriban shilingi milioni 6.5 za kenya kutoka kwa shirikisho la riadha Ulimwenguni.

Share This Article