Aliyekuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 68, chama chake kimesema.
Kulingana na Lungu chama hicho cha Patriotic Front (PF), Lungu alikuwa akipokea matibabu katika kituo kimoja cha Afya Jijini Pretoria, Afrika Kusini.
“Lungu amekuwa akipokea matibabu maalum nchini Afrika Kusini” kwa ugonjwa ambao haujatajwa, kilisema chama hicho kupitia kwa taarifa.
Mwana wake wa kike Tasila Lungu-Mwanasa, alisema babake amekuwa akitibiwa katika wiki za hivi karibuni, akidokeza kuwa matibabu hayo yalipata usaidizi kutoka kwa wasamaria wema.
Lungu, ambaye alikuwa mwanajeshi na wakili, alikuwa rais wa sita wa taifa hilo, alichukua uongozi mwaka 2015 baada ya mtangulizi wake Michael Sata kufariki akiwa afisini.
Lungu aliongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia 2015, na kushindwa katika uchaguzi na Rais wa sasa Hakainde Hichilema kwa kura nyingi.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi huo alijiondoa kwenye siasa lakini baadaye akarejea na kuonekana kuwa na nia ya kugombea tena urais.