Wingu la simanzi lilitanda katika kijiji cha Simat katika Kaunti ya Uasin Gishu, baada ya mwili wa jamaa aliyetoweka katika hali tatanishi kupatikana kando ya Mto Sosiani.
Mwili huo ambao baadaye ulitambuliwa kuwa wa Edwin Kiplimo Samoei wa miaka 29, ulipatikana baada ya mwendazake kutafutwa tangu tarehe 27 mwezi jana, aliporipotiwa kupotea.
Kisa hicho kimelaaniwa vikali na wakuu wa usalama wa eneo hilo nao watu wa tabaka mbalimbali wakitaka uchunguzi wa kina kufanyika.
Mwili huo ulipelekwa katika makavazi kwa upasuaji huku polisi wakiwataka wananchi wenye habari ya kisa hicho kutoa taarifa kwa polisi ili kufanikisha uchunguzi.
Taarifa za kisa hicho zinajiri wakati ambapo hali ya usalama imekuwa tete katika sehemu kadhaa nchini ambapo watu wengi wameripotiwa kupotea kisha baadhi yao kupatikana wamefariki.