Dorcas Rigathi: Ni jukumu la kila mtu kufanya maamuzi sahihi

Tom Mathinji
2 Min Read
Mkewe naibu Rais Dorcas Rigathi.

Mkewe naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi, amefungua kambi ya siku mbili ya matibabu inayolenga waraibu wa pombe na mihadarati katika eneo la Shimanzi, kaunti ya Mombasa.

Kwenye hotuba yake, mchungaji Dorcas alisema ni jukumu la kila mtu katika jamii kutafakari kuhusu maisha yao usoni na kufanya maamuzi sahihi.

“Nyingi ya familia zetu zimeathirika. Wakati umewadia wa kukabiliana na uraibu huu. Hatuwezi kama taifa kutofanya lolote, na kutarajia kwamba kuna mtu atakuja kutuokoa,”alisema mhubiri Dorcas.

Aidha mchungaji Dorcas alisifu mpango alioanzisha wa urekebishaji tabia, unaojumuisha wanaume 65 katika kaunti ya Meru, wengine 82 kaunti ya Nairobi, 50 eneo la Limuru na makumi ya wengine wanaojihusisha na upanzi wa miti katika eneo bunge la Mathira.

“Lazima tuchukue uamuzi wa kujiokoa. Nchini Kenya asilimia 75 ya idadi ya watu ni wa chini ya umri wa miaka 35. Iwapo tutatafakari kuhusu siku za usoni, utatambua ni kwanini tuna uamuzi wa kutekeleza,” alidokeza mchungaji Dorcas.

Naibu kamishna wa kaunti ya Mombasa Ronald Mwiwawi, alidokeza kuwa changamoto kubwa inayowakabili familia zinazoishi mitaani ni ukosefu wa stakabadhi za utambulisho.

“Tangu Rais alipozuru eneo hili mwezi Mei, tuliwasajili watu 352, lakini tuligundua kuwa miongoni wao, watu 272 hawakuwa na vitambulisho. Stakabadhi hiyo ni muhimu ili kupata ajira,”alisema Mwiwawi.

Website |  + posts
Share This Article