Mfalme Willem-Alexander na Malkia Maxima wa uholanzi ambao waliwasili hapa nchini Jumatatu usiku, leo Jumanne wanatarajiwa kuwa na shughuli kadhaa, kulingana na ratiba iliyotolewa.
Saa za asubuhi, Rais William Ruto na Mama Taifa Rachel Ruto watawaalika rasmi viongozi hao wa uholanzi katika Ikulu ya Nairobi, kabla ya kushiriki mazungumzo, utakaohudhuriwa na baadhi ya mawaziri. Baadaye Mfalme huyo atawahutubia wanahabari.
Mfalme Willem- Alexander, kisha atatia saini Mkataba wa Maelewano na Kenya kuhusu Utalii, Biashara, Usalama, Kilimo na Uvuvi.
Atakamilisha ratiba ya asubuhi kwa kuzungumza na vijana, ikizingatiwa kuwa asilimia 75 ya idadi ya watu Kenya wana umri chini ya miaka 35. Mazungumzo hayo yataangazia haki za kibinadamu nchini Kenya, uongozi bora na demokrasia.
Ratiba ya alasiri ya Mfalme huyo na Malkia, watashiriki upanzi wa miti Jijini Nairobi, huku wakizungumza na jamii za eneo lililo karibu na msitu ambao wanajukumu muhimu katika utunzaji wa misitu.
Watahudhuria kongamano la kibiashara, litakaloangazia uhusiano imara katika ya Kenya na Uholanzi. Zaidi ya wafanyabiashara 50, taasisi na Mashirika yasiyo ya serikali yatahudhuria kongamano hilo kuhusu ustawishaji kilimo na Maji.
Katika kongamano hilo Mfalme huyo na Malkia watajadili ushirikiano muhimu kati ya Kenya na Uholanzi kuhusu uvumbuzi, Kilimo, uchukuzi, afya, nishati na maji.
Kisha atakamilisha ratiba ya Jumanne watakapoandaliwa dhifa ya jioni na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi.