Rais William Ruto amekiri kwamba kifo cha waziri mkuu wa zamani Raila Amolo Odinga ni pigo kubwa kwake, wanavyosema waandishi wa habari nchini.
Ikumbukwe kwamba Raila Odinga ndiye alimsaidia Rais Ruto kurejesha utulivu wa kisiasa nchini baada ya maandamano ya vijana na hivyo kusababisha kuundwa kwa serikali jumuishi almaarufu “Broadbased Government”.
Akihutubia waombolezaji huko Bondo leo, Rais Ruto alisimulia jinsi alipata habari za kifo cha Raila na alivyosimamia shughuli yote ya kurejesha mwili wa Raila nchini Kenya.
Rais alisema alipata ujumbe kutoka kwa Dkt. Oburu kwamba nduguye alikuwa amezidiwa na ugonjwa. Dakika 10 baadaye Oburu akampigia simu kumfahamisha kwamba Baba Raila ameaga dunia.
Baada ya kujadiliana na familia, Rais anasema aliwasiliana na serikali ya India kufanikisha uwasilishaji wa mwili wa mwendazake.
Jioni alipopanga viongozi kwenda kuchukua mwili wa Raila, Winnie Odinga alimlalamikia Rais akishangaa ni kwa nini ndege ya viongozi hao ilikuwa inaelekea Mumbai nchini India badala ya Kochi walikokuwa.
Lakini serikali ya India iliusafirisha mwili huo kwa ndege hadi Mumbai ambapo ulipokezwa ujumbe kutoka Kenya na safari ikaanza.
Kulingana na kiongozi wa nchi, yeye na Raila wamekuwa wakijadiliana kwa kina katika muda wa miezi mitatu iliyopita ambapo walikubaliana kwamba wajibidiishe watoe Kenya katika kiwango cha taifa linalokua hadi taifa lililostawi.
Ruto anasema Raila ndiye alitoa wazo la kumwalika Dkt. Hino nchini Kenya kujadiliana naye kuhusu jinsi ya kuendeleza suala hilo la kufanya Kenya kuwa bora.
