Rais William Ruto ametangaza kwamba atafanya ziara ya kikazi katika nchi jirani ya Uganda wiki ijayo.
Ruto aliyasema hayo alipokuwa akihutubia wakazi wa kaunti ya Homabay kwenye siku yake ya pili ya ziara ya kikazi ya siku nne katika kaunti za eneo la Nyanza.
Alikuwa akizumgumzia usalama katika mpaka wa Kenya na Uganda hasa katika ziwa Viktoria ambapo wavuvi wa Kenya hukamatwa mara kwa mara na polisi wa Uganda kwa kile kinachosemekana kuwa kuvua samaki kwenye maji ya Uganda katika ziwa hilo bila idhini.
Kiongozi wa taifa alisema mazungumzo kati yake na Rais Yoweri Museveni yamepangiwa kuandaliwa Oktoba 10, 2023 na suala la usalama wa wavuvi wa Kenya ni mojawapo ya masuala ambayo watajadili.
Gavana wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga, alimwomba Rais Ruto aingilie kati na kutatua matatizo ya wavuvi.
Nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zina himaya kwenye ziwa Viktoria na inakisiwa kwamba kupungua kwa samaki humo ndiko kunasababisha mizozo ya kila mara huku wavuvi wa nchi zote waking’ang’ania zilizopo.
Kisiwa cha Migingo hasa ndicho kinazozaniwa na Kenya na Uganda ambazo zote zinadai umiliki wake. Maji yaliyo karibu na kisiwa hicho yanasemekana kuwa na samaki wengi ikilinganishwa na sehemu nyingine za ziwa Viktoria.
Wengi wa wakazi wa kisiwa hicho ni wakenya.