Gavana wa California amesema amearifiwa kuwa wanajeshi 2,000 zaidi watatumwa mjini Los Angeles kufuatia siku kadhaa za makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama kuhusu misako ya kuwakamata wahamiaji.
Hilo limethibitishwa na utawala wa Trump.
Msemaji mkuu wa Ikulu ya Marekani Sean Parnell amethibitisha kuwa walinzi wengine wanapelekwa mjini humo.
“Kwa agizo la Rais, Idara ya Ulinzi inakusanya Walinzi wa Kitaifa wa ziada 2,000 wa California kuitwa katika huduma ya usalama ya taifa kuwezesha maafisa wa kutekeleza sheria kwa ajili ya udumishaji usalama,” Parnell alisema.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisisitiza kutumwa kwa wanajeshi kukabiliana na maandamano ya kupinga uvamizi wa wahamiaji huko LA.
“Utawala huu hautatishwa na uvunjaji sheria,” Vance alisema. “Rais Trump hatarudi nyuma.”
Hata hivyo Gavana Gavin Newsom ameitaja hatua hiyo ya Trump kuwa ni kutimiza ndoto ya rais dikteta huku mwanasheria mkuu wa California akimshitaki Rais Trump kwa kutuma majeshi jimboni humo bila ya ridhaa ya Gavana.