Rais Ruto: Maandamano hayatafanyika wiki ijayo

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto amesema serikali yake haitakubali maandamano yoyote kufanyika nchini wiki ijayo.

Kauli zake zinawadia wakati ambapo muungano wa Azimio umetangaza kuwa utafanya maandamano siku za Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo.

“Mimi nataka niwaambie, maandamano haiwezi tena kufanyika katika taifa hili letu la Kenya. Hiyo wanasema Wednesday, hiyo wanasema sijui lini, hiyo maandamano haiwezekani. Haiwezekani,” alionya Rais Ruto wakati akiwahutubia raia wakati wa uzinduzi wa barabara ya Njabini kuelekea Naivasha katika kaunti ya Nakuru.

“Walifanya maandamano Ijumaa iliyopita ile ingine watu saba wakakufa. Wamefanya maandamano juzi, watu nane wakakufa.”

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa, muungano Azimio ulitangaza kuwa umeamua kuongeza idadi ya siku za maandamano kutokana na shinikizo kutoka kwa umma.

“Kuanzia sasa, maandamano ya amani sasa yatafanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo kutokana na maombi mengi kutoka kwa umma ya kuongeza kasi ya maandamano,” ulisema muungano wa Azimio katika taarifa yake.

Muungano huo ulitangaza hayo wakati taarifa za polisi zikiashiria kuwa idadi ya waliofariki kutokana na maandamano ya Azimio watu 17, baada ya mili mingine minne kupatikana katika kaunti ya Nairobi.

Miongoni mwa walioangamia ni bingwa wa mashindano ya ndondi ya Nairobi Open katika uzani wa Bantam Raphael Shigali aliyekumbana n amauti baada ya kujipata katika kundi la watu waliokuwa wakitoroka polisi mtaani Hamza alipofyatuliwa risasi.

Mtu mmoja pia ameripotiwa kufariki katika mtaa wa Mukuru, alipogongwa na mkebe wa kitoa machozi kifuani akitoka katika kituo kimoja cha afya.

Mtaani Majengo, wakazi walipeleka mwili wa mwanamume mmoja katika kituo cha polisi huku mwili huo ukiwa na majeraha ya kudungwa kisu.

Watu wengine wawili zaidi wameripotiwa kufariki kaunti ya Kisumu kutokana na maandamano.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *