Rais William Ruto hivi leo amezindua kituo kidogo cha kuzalisha umeme cha Kimuka katika eneo bunge la Kajiado Magharibi kaunti ya Kajiado.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, kiongozi wa nchi alisema kituo hicho kitaimarisha usambazaji umeme katika eneo hilo huku kikiondolea kituo kidogo cha kuzalisha umeme cha Nairobi Kaskazini mzigo wa kusambaza megawati 80 za umeme.
Huku akisisitiza kwamba mpango wa uunganishaji stima mashinani almaarufu “last mile electricity connectivity” ni mojawapo ya ile iliyopatiwa kipaumbele na serikali yake, Rais alisema kwamba lengo ni kupiga jeki biashara.
Kituo hicho cha Kimuka kinatarajiwa pia kupunguza matatizo ya kukatika kwa umeme kila mara, kuhakikisha uwepo wa umeme wakati wote na usambazaji wa kutegemewa wa umeme.
Kitatoa huduma za umeme kwa watu laki 6, wakazi wa maeneo ya Karen, Dagoretti, Kikuyu, Kabete, Ngong, Matasia, Magadi na Ngemwa.
Kuhusu joto la kisiasa nchini, Rais Ruto aliwataka wanaotilia shaka uongozi wake wasubiri mwaka 2027 wakati wa uchaguzi mkuu kama aliongoza vyema wamwongezee muhula mwingine uongozini na kama hatakuwa amefanya vyema watekeleze haki yao ya kikatiba.