Ruto asema walimu wa JSS watapatiwa ajira ya kudumu

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametoa hakikisho kwamba walimu wa shule za Sekondari Msingi au Junior Secondary School, JSS wataajiriwa kwa masharti ya kudumu.

Kiongozi wa nchi ambaye alizungumza kwenye mahojiano na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi jana Jumapili usiku, alifafanua kwamba walimu hao watabadilishiwa masharti baada ya miaka miwili ya uanagenzi.

Kulingana naye, ni mpango wa serikali sasa kwamba kila mwalimu anayejiunga na huduma humu nchini sharti ahudumu kwa masharti ya mkataba kwa muda wa miaka miwili kabla ya kuajiriwa kwa masharti ya kudumu.

Kiongozi wa nchi alisema walimu hao ambao wamehudumu kwa muda wa mwaka mmoja, wataendelea kuhudumu kwa mwaka mwingine mmoja kuanzia mwezi Januari kisha baadaye wapate ajira ya kudumu.

Alisema pia kwamba mpango huo wa kuhudumu chini ya mkataba kama mwanagenzi unaanzishwa katika sekta nyingine za utendakazi serikali kwani hiyo ndiyo njia ya kujifahamisha kazi kabla ya kupata ajira ya kudumu.

Walimu wa JSS ambazo zimekuwepo kwa mwaka mmoja sasa wamekuwa wakilalamika wakitaka kubadilishiwa masharti ya ajira ili iwe ya kudumu wakisema wao ni walimu kamili.

Mwanzo wa mwezi Disemba, wawakilishi wa walimu hao walifanya mkutano na wanahabari kwenye afisi za chama cha walimu wa shule za sekondari na taasisi za elimu ya juu KUPPET jijini Nairobi.

Walisema wakati huo kwamba wanachotaka shule zitakapofunguliwa Januari 2024, ni barua za kuwaanzishia ajira ya kudumu lakini inaonekana huenda wakasubiri kwa muda zaidi.

Share This Article