Rais William Ruto amemteua Adan Mohamed kuwa afisa mkuu mtendaji wa kitengo cha utekelezaji wa miradi ya serikali.
Awali, Adan alikuwa mwanachama wa baraza la rais la washauri wa kiuchumi, linaloongozwa na Dkt. David Ndii.
Adan, aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa Viwanda na Ustawi wa Biashara katika serikali iliyopita, sasa atasimamia afisi ya mipango ya Rais ya utekelezaji wa ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza.
Uteuzi wake uko kwenye agizo la Rais Nambari 2 lililotolewa leo Alhamisi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.
Katika agizo hilo, Rais Ruto pia ameongeza majukumu ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ambaye kwa ushirikiano na mawaziri na makatibu wa wizara, atasimamia utawala wa mashirika yote ya serikali na taasisi za umma.
Vile vile kufuatia agizo hilo, afisi ya Waziri mwenye Mamlaka Makuu pia imepanuliwa ili kujumuisha idara mbili za serikali kwenye wizara ya mashauri ya nchi za kigeni.