Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, ameunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, akisema amefanikisha kwa usawa miradi ya maendeleo katika pembe zote za taifa hili.
Dkt. Omollo alisema serikali imeipa sekta ya uvuvi umuhimu mkubwa, kupitia uwekezaji wa miundombinu.
“Kwa mara ya kwanza, tunaye Rais anayetambua kuwa wavuvi wanahitaji kushughulikiwa kama vile wakulima wa Majani Chai, Kahawa, miwa na bidhaa zingine. Maendeleo ya taifa hili ni sharti yawanufaishe Wakenya wote.
Aidha, alitaja ujenzi wa vituo vya kushughulikia samaki, masoko na vifaa vya kuhifadhi samaki katika kaunti zilizo karibu na ziwa Victoria, akisema imeimarisha sekta ya uvuvi, kupunguza hasara baada ya mavuno na kuongeza mapato kwa jamii ya wavuvi.
Aliyasema hayo alipokutana na wasimamizi wa ufuo, waliowakilisha fuo 20 katika eneo bunge la Budalangi, kaunti ya Busia.
Kulingana na Omollo, uchumi samawati awali uliathirika pakubwa kutokana na ukosefu wa uwekezaji licha ya kuwa na uwezo wa kubuni nafasi za ajira, kuimarisha maisha na kuchangia kwa utoshelevu wa chakula nchini Kenya.
Kuhusu usalama wa majini, katibu huyo alielezea mipango ya kuongeza idadi ya maafisa wa ulinzi wa majini katika kaunti ya Busia ili kuimarisha usalama wa wavuvi.
“Wavuvi wetu wanapaswa kutekeleza shughuli zao bila uwoga wa kuhangaishwa au ukosefu wa usalama,” alidokeza Omollo.
Omollo aliwaagiza Machifu, Manaibu wao na Maafisa wa Serikali Kuu, kutandaa mikutano ya mara kwa mara na wakazi ili kushughulikia maswala yao na pia kuwafahamisha kuhusu mipango ya serikali.