Hassan Omar Daffa ateuliwa Kadhi Mkuu

Uteuzi wa Daffa ulitekelezwa baada ya kukamilika kwa mchakato ulioanza Januari 16, 2026, wakati ambapo JSC ilitangaza nafasi hiyo kuwa wazi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Hassan Omar Daffa ateuliwa Kadhi Mkuu.

Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama  (JSC), imemteua Hassan Omar Daffa kuwa Kadhi Mkuu, kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha  Sheikh Abdul Halim Hussein.

Awali Daffa alishikilia wadhifa wa Kadhi Mwandamizi huku akiwa na shahada ya Sharia na somo la dini ya Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Umm Al-Qura nchini Saudi Arabia.

Aidha, ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya, na pia ni wakili katika Mahakama Kuu ya Kenya.

Kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, Jaji Mkuu Martha Koome ambaye ni mwenyekiti wa  JSC, alisema Kadhi Mkuu huyo mpya analeta tajiriba na falsafa ya Kiislamu na huduma za idara ya mahakama.

Uteuzi wa Daffa ulitekelezwa baada ya kukamilika kwa mchakato ulioanza Januari 16, 2026, wakati ambapo JSC ilitangaza nafasi hiyo kuwa wazi.

JSC ilipokea maombi 14 kwenye wadhifa huo, huku ikiwaorodhesha wawaniaji 9, ambao walisailiwa kati ya Novemba 2 na 3, 2026.

Kadhi Mkuu husimamia  mahakama zote za kadhi kote nchini, ambazo hushughulikia kesi za dini ya kiislamu ikiwa ni pamoja na maswala ya ndoa, talaka, urithi na yale ya kibinafsi.

Share This Article