Rais Ruto aangazia mpango wa nyumba za bei nafuu Eldoret

Alizungumza na msichana wa miaka 21 kupata nyumba ya chumba kimoja katika mradi wa Pioneer Affordable Housing mjini Eldoret.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Kenya, William Ruto, ameangazia athari za mpango wa serikali wa nyumba za bei nafuu katika mkutano alioandaa na wakazi wa Eldoret.

Hii ni baada ya Abigail Chepkemboi, mwanafunzi wa uhandisi wa umeme wa umri wa miaka 21, kupata nyumba ya chumba kimoja katika mradi wa Pioneer Affordable Housing mjini Eldoret.

Ruto alisema mafanikio ya Abigail yanaakisi lengo la serikali yake la kuwezesha Wakenya kumiliki nyumba bora, ambao vinginevyo wangepata ugumu wa kumudu gharama za ununuzi wa nyumba.

Rais alitoa kauli hiyo baada ya kuzindua rasmi mradi wa Pioneer na kuzungumza na wanufaika mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alibainisha kuwa miradi mingine ya nyumba imepangwa katika kaunti hiyo, ukiwemo mradi nyumba 2,231 katika mji wa Eldoret Railway City, nyumba 1,800 huko Kidiwa awamu ya pili na nyumba 2,000 katika mradi wa Lumumba.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, nyumba 12,429 za bei nafuu za thamani ya shilingi bilioni 29.9 za Kenya zimepangwa kujengwa au zinaendelea kujengwa katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika kaunti hiyo, unaojumuisha mabweni ya wanafunzi na masoko ya kisasa, unafikia shilingi bilioni 41.8.

Kitaifa, Rais alisema takribani nyumba 300,000 zinaendelea kujengwa huku serikali ikiendeleza mpango wake wa kuhakikisha Wakenya wanapata makazi ya bei nafuu.

Share This Article