Rais azindua kiwanda cha simu za rukono EADAK

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo amezindua kiwanda cha kuunda simu za kisasa katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos.

Kiwanda hicho kwa jina East Africa Device Assembly Kenya – EADAK kinaendeshwa na kampuni na mawasiliano ya simu za rununu Safaricom.

Rais alisema kwa sababu ilikuwa ajenda yake kuhakikisha kila mkenya anaonja utamu wa sekta ya dijitali aliamua kuwekeza katika uundaji wa vifaa hitajika ambavyo ni simu za rununu nchini.

Alishukuru wawekezaji ambao pia wamewekeza kwenye mpango huo huku akiahidi kwamba serikali itaongoza katika kuwa mteja wa bidhaa zinazoundwa kwenye kiwanda hicho.

Alisema tayari ametekeleza ahadi hiyo kupitia wizara ya afya ambayo ilinunua simu za rununu laki moja zitakazotumiwa na wahudumu wa afya ya jamii.

Rais alizindua pia simu za kwanza za bei nafuu zilizoundwa na EADAK.

Rais Ruto akiwa ameshika mojawapo ya simu zilizoundwa na EADAK

Eliud Owalo ambaye ni waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali alisema leo ni siku muhimu kwa nchi ya Kenya kwa sababu ndoto ya upatikanaji wa vifaa vya kidijitali vya bei nafuu imetimia.

Waziri wa afya Susan Nakhumicha aliyezungumza kwenye hafla hiyo ya uzinduzi alijivunia kuwa mteja wa kwanza wa kiwanda cha EADAK.

Kiwanda hicho ndicho kiliunda simu za rununu ambazo wahudumu wa afya wa jamii walipatiwa kutumia kazini na ziko na mfumo wa ukusanyaji data ambao pia ulitayarishwa na EADAK kwa jina “electronic Community Health Information System – eCHIS.

Kulingana naye, mfumo huo ulipunguza pakubwa idadi ya faili ambazo wahudumu hao walikuwa wakibeba wakienda nyanjani na umeharakisha ukusanyaji data.

Website |  + posts
Share This Article