Shambulizi la Westgate: Miaka 10 baadaye

Martin Mwanje
2 Min Read

Inatimia miaka 10 leo Alhamisi tangu kutokea kwa shambulizi la kigaidi katika jumba la Westgate mtaani Westlands, jijini Nairobi. 

Watu 67 walifariki wakati wa shambulizi hilo lililodumu siku nne na ambalo kundi la wanamgambo la Al-Shabaab lilidai kutekeleza.

Manusura kadhaa wa shambulizi hilo waliachwa wakiuguza majeraha na makovu ya walichokishuhudia siku hiyo bado yanawaandama.

“Daima, mioyo yetu itasalia kuwa mizito ikijawa na kumbukumbu za wale tuliowapoteza, na hii leo, tunawakumbuka na kusimama pamoja na familia zao zinazoomboleza, tukishirikishana uzito wa vifo visivyofikirika vilivyotokea,” amesema Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa, Dkt. Raymond Omollo.

“Matukio yanayohusiana na shambulizi hilo yalitikisa nchi yetu na kuacha kumbukumbu isiyoweza kufutika. Lakini zaidi ya hilo, yaliyotokea baadaye ni ushuhuda wa uimara na uthabiti wetu, na yalitupa mafunzo yenye thamani sana juu ya kukaa chonjo, kujiandaa, kuitikia hali za dharura na umuhimu wa kutohadhari  kamwe dhidi ya tishio lolote la usalama wetu wa umma.”

Dkt. Omollo anasema nchi ya Kenya inaimarisha uwezo wake taratibu kupitia kuajiriwa kwa maafisa zaidi wa usalama, kuanzishwa kwa vikosi maalum, utoaji wa programu za kisasa za mafunzo kwa maafisa wa usalama na uimarishaji wa uwezo wa kupiga silaha kama inayoelezwa katika Mpango wa Kuwapa Polisi Silaha za Kisasa.

“Lengo letu hatimaye ni kuendeleza uangalizi wa kiwango cha juu kwenye mipaka yetu na operesheni za usalama za kisiri na za wazi kote nchini na kumwangamiza adui kabla ya kutokea kwa mashambulizi,” amesema Dkt. Omollo katika taarifa ya kuadhimisha miaka kumi tangu kutokea kwa shambulizi hilo.

Ameongeza kuwa Kenya inaendelea kukuza ushirikiano wa kimkakati na washirika wake duniani katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa pamoja dhidi ya ugaidi.

Katibu huyo ameilimbikizia sifa sekta ya ulinzi ya kibinafsi kwa kutekeleza wajibu mkubwa katika kupiga jeki juhudi za serikali kutoa ulinzi kote nchini, akiongeza kuwa mipango ya kuimarisha sekta hiyo tayari imeanzishwa.

Website |  + posts
Share This Article