Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, amegoma kuhusika katika kusikilizwa kwa kesi ya uhaini dhidi yake katika mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Hii ni baada ya uongozi wa mahakama kuamua kuendesha kesi hiyo, iliyosubiriwa kwa hamu, kupitia mtandao badala ya Lissu kufikishwa mahakamani moja kwa moja.
Askari wa magereza aliyezungumza kutoka gereza la Ukonga kwa njia ya video alielezea kwamba Lissu alikataa kuingia kwenye chumba ambacho kilikuwa kimetengwa kwa ajili ya uunganishaji wa kimtandao ili kusikiliza kesi dhidi yake.
Lissu badala yake alitaka apelekwe katika mahakama ya Kisutu ambapo viongozi kadhaa wa chama chake pamoja na raia walikuwa wamejitokeza kufuatilia kesi hiyo.
Hata hivyo, hakimu mkazi mwandamizi anayeshughulikia kesi hiyo Godfrey Mhini aliruhusu kesi hiyo iendelee bila uwepo wa Lissu ambaye anawakilishwa na mawakili takribani 28 akiwemo Peter Kibatala.