Maelfu ya watu walijitokeza Ijumaa jioni kuwasha mishumaa katika bustani ya Uhuru Jijini Nairobi, kumbukuba aliyekuwa kiongozi wa chama cha ODM hayati Raila Odinga.
Raila alifariki Oktoba 15, 2025 alipokuwa akipokea matibabu nchini India.
Hafla hiyo ya kuwasha mishumaa na ambayo pia ilitekelezwa katika sehemu zingine za nchi, inaashiria mwanzo wa mwezi mzima wa kumuenzi Raila almaarufu Mwezi wa Baba, kabla ya maadhimisho ya kwanza ya kifo chake tarehe 15 mwezi huu wa Oktoba.
Hafla kwenye bustani ya Uhuru Park ilianza mwendo wa saa tisa huku maonesho ya muziki na densi yakitangulia tukio la kuwasha mishumaa.
Wafuasi wa hayati Raila Odinga waliwasili wakibeba mishumaa, mashada ya maua na picha za kiongozi huyo huku wasanii mbalimbali wakijitokeza kumuenzi katika hafla hiyo.
Matukio sawa na hayo ya uwashaji mishumaa yaliandaliwa kwenye eneo la Treasury Square jijini Mombasa, Nakuru na Kisumu kama sehemu ya mpango wa kumbukizi za kitaifa.
Jijini Nairobi, wasifu wa kiongozi huyo na sera zake za uongozi ulioneshwa kupitia projekta kwenye jumba la mikutano ya kimataifa la KICC kuanzia saa moja usiku.