Shirika la Umoja wa Mataifa limesema Haiti inaendelea kukabiliwa na janga kubwa la usalama na haki za binadamu, huku magenge ya wahalifu wenye silaha yakienea huku raia wakikosa huduma muhimu.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema, raia nchini Haiti wamenaswa katikati ya vita vya magenge wenye silaha na vikosi vya usalama, akidokeza kuwa afisi yake imenakili takriban watu zaidi ya 5,000 ambao wamefariki na kujerehiwa mikononi mwa magenge na operesheni za kiusalama kati ya Januari 1 na Septemba 11,2026.
Akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha 63 cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswizi, Turk aliongeza kuwa takriban watu 230 wametekwa nyara, na wanawake 1,000 wamebakwa.
Kulinagana na Türk, licha ya vikosi vya usalama kupata mafanikio katika kudhibiti baadhi ya shughuli za magenge katika maeneo ya mji mkuu Port-au-Prince, makundi hayo yanaendelea kubadilisha mbinu, na kupanua wigo wa maeneo yao.
Mashambulizi ya hivi karibuni katika maeneo ya Kenscoff na Gressier, pamoja na kuongezeka kwa uwepo wa magenge katika eneo la Sud-Est, yanaashiria mkakati wa kutwaa maeneo mapya na njia muhimu za uchukuzi.
Mkuu huyo wa Haki za Binadamu amesema hali hiyo inatishia utulivu nchini Haiti na maeneo ya jirani.
Ameeleza kuanza kwa operesheni za Kikosi cha Kudhibiti Magenge ya uhalifu, kilichoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuwa ni hatua iliyosubiriwa kwa muda mrefu kuelekea usalama zaidi.
Hata hivyo, amesema kikosi hicho bado kiko chini sana ya nguvu kinachohitajika kuwa nayo na ametaka kipelekwe kikamilifu na kwa haraka, huku kikihakikisha ulinzi madhubuti wa haki za binadamu.