Polisi wanasa sigara bandia Kiambu

Kwenye msako wa kijasusi, maafisa hao walipata aina tofauti za sigara na mihuri ghushi ya Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA).

Tom Mathinji
1 Min Read
Polisi wanasa sigara bandia Kiambu.

Maafisa wa Polisi wamenasa mtandao unaoshukiwa kuhusika katika usambazaji sigara bandia katika kaunti ya Kiambu.

Kwenye msako wa kijasusi, maafisa hao walipata aina tofauti za sigara na mihuri ghushi ya Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA).

Operesheni hiyo ilimlenga mfanyabiashara Patrick Muiruri Mwangi, anayeshukiwa kuhusika katika biashara hiyo haramu ya uuzaji na usambazaji wa sigara ambazo hazijalipiwa ushuru na zilizouzwa kwa njia ya kimagendo.

Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walianza uchunguzi kwenye majengo mawili yanayohusishwa na mfanyabiashara huyo, wakifuatilia kwa karibu mienendo na shughuli zake.

“Maafisa walivamia majengo hayo na baada ya upekuzi walipata sigara hizo pamoja na mihuri za KRA zinazoshukiwa kuwa ghushi,” ilisema DCI kwenye ukurasa wa X.

Hata hivyo mshukiwa huyo alitoroka na sasa anatafutwa na polisi ili afunguliwe mashtaka.

TAGGED:
Share This Article