Raia waandamana Niger wakitaka balozi wa Ufaransa aondoke

Marion Bosire
1 Min Read
Anti-sanctions protestors gather in support of the putschist soldiers in the capital Niamey, Niger August 3, 2023. REUTERS/Balima Boureima NO RESALES. NO ARCHIVES

Raia wengi ambao wanaunga mkono mapinduzi ya hivi maajuzi ya serikali ya nchi hiyo, waliandamana katika jiji kuu Niamey wakiitaka Ufaransa iondoe balozi wake na wanajeshi wake nchini humo.

Haya yanafuatia madai ya viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwamba wafaransa hao wanaingilia masuala ya nchi yao.

Waandamanaji walikusanyika nje ya kambi ya kijeshi ambayo inakaliwa na wanajeshi wa Ufaransa baada ya wito uliotolewa na makundi kadhaa ya utetezi ambayo yanaunga mkono mapinduzi.

Utawala wa kijeshi nchini Niger uliochukua mamlaka Julai 26, 2023, umemlaumu Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kutumia mbinu za matamshi ya kuleta mgawanyiko anapozungumzia mapinduzi ya Niger huku akijaribu kuanzisha uhusiano wa kikoloni na koloni hiyo yake ya zamani.

Macron anaunga mkono Rais aliyebanduliwa madarakani Mohamed Bazoum na amekataa kutambua serikali ya kijeshi.

Sylvain Itte, balozi wa ufaransa nchini Niger, ameendelea kusalia nchini humo hata baada ya makataa ya kuondoka ya saa 48 kukamilika, uamuzi ambao Macron anaunga mkono.

Share This Article