Mwanasiasa na mwanamuziki wa Tanzania Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay ametangaza uzinduzi wa wakfu wake kwa jina “Profesa Jay Foundation” Novemba 24, mwaka huu wa 2023.
Haya yalifichuliwa na mke wa Prof Jay Grace Mgonjo aliyekuwa akihojiwa kwenye kipindi cha “Leo Tena” cha kituo cha redio cha Clouds FM nchini Tanzania.
Grace ambaye amekuwa kwenye ndoa na Jay kwa miaka 6 na kwenye mahusiano naye kwa jumla ya miaka 17, alielezea kwamba, wakfu huo utakuwa ukishughulikia masuala ya afya ya figo.
Figo ya mwimbaji huyo iliathirika baada yake kuugua kwa muda mrefu shindikizo la damu na Corona. Kwa sasa yeye huwa anahudhuria matibabu ya figo almaarufu “Dialysis”.
Kando na hayo, Grace alisema Jay yuko sawa isipokuwa hivi maajuzi alivunjika mguu akielekea kwenye ATM kutoa pesa lakini akasisitiza kwamba yuko sawa kiafya.
“Alikuwa amekwenda kutoa pesa kwenye ATM, mtu akaja kuegesha gari kwa kishindo akamshtua akaanguka, lakini yuko sawa.” alisema Grace.
Mwanzo wa mwaka 2022, Jay aligonjeka na kulazwa kwenye hospitali ya Muhimbili ambako alikuwa amepoteza fahamu.
Umma ulifahamu kuhusu kuugua kwa mwanamuziki huyo baada ya familia yake kujitokeza na kuomba msaada wa fedha ili kugharamia matibabu yake.
Mke huyo wa Jay alisema sauti ya mume wake ipo ila sio nzuri kama awali ikitizamiwa kwamba alifanyiwa upasuaji ambao kidogo uliathiri sauti.
Alisimulia alivyofurahi wakati mume wake alipata fahamu lakini akawa amesahau kila kitu na ikabidi wawe wakimfahamisha kuhusu matukio mbali mbali.
“Kumbukumbu zilirejea tulipotoka India kwa matibabu” alisema Grace huku akielezea kwamba sasa Jay anaelewa na kukumbuka kila kitu.
Grace anasema wamechochewa kuanzisha wakfu huo baada ya kuona matatizo ambayo wagonjwa wa figo walikuwa wanapitia ili kupata matibabu.