Portable ahukumiwa kifungo cha miezi mitatu gerezani

Hukumu hii inatokana na makosa aliyotekeleza mwaka 2022 katika jimbo la Ogun.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria mwenye utata Habeeb Okikiola maarufu kama Portable amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu gerezani na mahakama moja ya Abeokuta, jimbo la Ogun.

Mahakama ilipata kwamba mwimbaji huyo ana hatia kwenye makosa mawili ya kushambulia afisa wa polisi na kukataa kukamatwa na anaweza kukwepa muda gerezani kwa kulipa faini ya Naira elfu 30.

Mwanamuziki huyo alikamatwa mwezi Machi mwaka 2023 kwa kishambulia Inspekta wa polisi na kuzuia maafisa wa polisi waliokuwa wakimwasilishia na kutekeleza kibali cha kumkamata.

Inspekta wa polisi Olumide Awoleke alifahamisha mahakama awali kwamba Portable alitekeleza makosa hayo Novemba 18, 2022, saa tano asubuhi katika eneo la Okeosa, Ilogbo, jimbo la Ogun.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, Portable alimpiga Osimosu Emmanuel Oluwafemi siku hiyo. Analaumiwa pia kwa kuiba ala za muziki.

Katika uamuzi wake, hakimu mkuu Babajide Ilo, alimpata Portable na hatia kwenye makosa mawili na hukumu ya kosa la kwanza ni kifungo cha mwezi mmoja gerezani au faini ya Naira elfu 10.

Kwa kosa la pili, mwanamuziki huyo alihukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani au faini ya Naira elfu 20.

Website |  + posts
Share This Article