Mwanamieleka Terry Gene Bollea ambaye wengi wanamfahamu kwa jina Hulk Hogan ametangaza ujio wa ligi yake ya mieleka ambayo ameipa jina la Real American Freestyle – RAF.
Hogan wa umri wa miaka 71 sasa alistaafu kutoka kwa mieleka mwaka 2012 baada ya kujipatia nafasi bora katika tasnia hiyo.
Ligi ya RAF ni ushirikiano kati ya Hogan, Eric Bischoff na kocha Israel Martinez.
Uzinduzi rasmi wa ligi hiyo unatarajiwa kuandaliwa Agosti 30, 2025 huko Cleveland na anatumai kwamba Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni rafiki yake atahudhuria.
Hii ni baada ya Hogan kuona Trump akihudhuria mashindano ya mieleka ya NCAA daraja ya Kwanza huko Philadelphia mwezi uliopita.
Katika mahojiano mwanamieleka huyo alisema atampigia simu Trump ili kumwalika.
Lakini hata bila uwepo wa Trump, Hogan amesema anatarajia makuu kutoka kwa ligi hiyo ambayo anasema itakuwa tofauti na mashindano mengine ya mieleka ambayo alijihusisha nayo awali.
Ligi ya RAF itahusisha mieleka ya ukweli ambayo haijapangwa na kutakuwa na vitengo vya wanaume na wanawake.
Katika tangazo lake Hogan alisema kwamba wanamieleka watalipwa kupiga wapizani wao na baadaye akaashiria kwamba mishahara yao itakuwa mikubwa.
Kulingana na Hogan yeye na wanabiashara wenzake walipata wazo la kuanzisha ligi hiyo ya mieleka wakati alianzisha kampuni yake ya kutengeneza bia ya Real American Beer company.