Maafisa wa usalama na utawala watakaopatikana wakikosa kuchukua hatua kali dhidi ya utengenezaji, uuzaji na unywaji wa pombe haramu kuanzia sasa watafutwa kazi.
Awali, maafisa hao waliendelea kuhudumu ila walihamishiwa maeneo mengine ya utawala kama adhabu.
Hata hivyo, Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki anasema ili kuongeza makali ya vita dhidi ya pombe haramu nchini, maafisa wa usalama na utawala watakaozembea kazini sasa watapigwa kalamu.
“Kama sera, maafisa wa usalama na utawala wanaowezesha utengenezaji, uuzaji na utumiaji wa pombe haramu na dawa za kulevya hawatahamishiwa maeneo mengine. Watafutwa kazi mara moja na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Prof. Kindiki leo Jumatatu katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Mombasa akiwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua na mawaziri wengine.
“Vile vile, maafisa wa usalama na utawala wanaofanya kazi maridhawa katika vita dhidi ya matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya watatambuliwa na kutunukiwa na serikali kupitia kupandishwa vyeo na kupewa tuzo za kitaifa.”
Matumizi ya pombe haramu nchini yamekuwa suala nyeti ambalo limesababisha maafa katika baadhi ya maeneo ya nchi, la hivi karibuni zaidi likiwa kaunti ya Kirinyaga.
Siku zilizopita, serikali imeapa kukabiliana vikali na matumizi ya pombe hiyo sawia na dawa za kulevya.
Hata hivyo, licha ya serikali kuahidi kuangamiza matumizi ya bidhaa hizo hatarishi, pombe haramu na dawa za kulevya zinasala kuwa mwiba unaosababisha maafa na madhara yasiyoelezeka ya kiafya kwa waraibu wake nchini.