Mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani Polo G ameachiliwa na maafisa wa polisi katika jimbo la Los Angeles.
Polo wa umri wa miaka 25 ambaye jina lake halisi ni Taurus Tremani Bartlett, aliachiliwa jana Jumatatu Oktoba 21, 2024, kwa mujibu wa ripoti kwenye tovuti ya maafisa hao wa usalama.
Alikamatwa Oktoba 19, katika eneo la San Fernando Valley, baada ya kusimamishwa na maafisa wa polisi kwa sababu ya kuendesha gari kwa kasi ya juu.
Polisi hao walitekeleza msako kwenye gari lake wakapata bunduki ambayo inasemekana kuwa na risasi ndani.
Kosa alilokamatwa kwalo ni kuficha silaha kwenye gari lakini katika kumwachilia huru, polisi walisema kwamba waliridhika kwamba hakukuwa na sababu za kutosha za kumfungulia mashtaka.
Msanii huyo anapangiwa kuanza ziara yake ya kikazi aliyoipa jina la “Hood Poet Tour” Oktoba 24, 2024.
Hii si mara ya kwanza kwa rapa huyo kupata matatizo ya kisheria mwaka huu. Alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumiliki bunduki mwezi Aprili mwaka huu, baada ya kuacha silaha kwenye chumba cha hoteli mjini New York, ambayo baadaye ilipatikana na mjakazi.
Polo alipatiwa dhamana kutokana na tukio hilo licha ya pingamizi kutoka kwa waendesha mashtaka, ambao walitaja rekodi ya uhalifu ya zamani ya rapa huyo ambayo ni pamoja na kukamatwa kwa utekaji nyara, shambulio na wizi.
Polo pia alikamatwa mwaka jana kwa kupatikana na bunduki kufuatia msako kwenye nyumba yake Kusini mwa California, ambapo alikamatwa pamoja na kakake Trench Baby, ambaye alishtakiwa kwa wizi.
Uvamizi wa makazi yake unadaiwa kutokana na ripoti ya awali kwamba Baby aliibia mwanamume mmoja huko Granada Hills wakati wa kunakili video za muziki.