PAC yakagua hesabu za Wizara ya Ardhi

Katibu Nixon Korir aliitwa kujibu masuala yaliyoibuliwa katika Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa Wizara ya Ardhi Nixon Korir alifika mbele ya Kamati ya Uhasibu ya Bunge, PAC kujibu masuala yaliyoibuliwa katika Ripoti ya Mkaguzi Mkuu kuhusu hesabu za serikali kuu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Kikao hicho kilifanyika katika majengo ya bunge na kuongozwa na mbunge wa Butere, Tindi Mwale, ikiwa ni sehemu ya jukumu la bunge la kusimamia uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma.

Wakati wa kikao hicho, Katibu Korir alijibu maswali kuhusu taarifa za kifedha za Idara ya Ardhi na Mipango ya Kimaeneo pamoja na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa ni kucheleweshwa kwa utekelezaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Taarifa za Ardhi,

ambapo ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ilibainisha kuwa kati ya sajili 83 za ardhi nchini, ni sajili za Nairobi na Murang’a pekee zilizokuwa zimekamilisha mchakato wa kidijitali.

Akijibu hoja hiyo, Korir  alisema mfumo huo umeanza kutekelezwa katika sajili za ardhi za Mombasa na Isiolo, huku maendeleo makubwa yakifikiwa Mombasa na Marsabit.

PAC ilihimiza Idara ya Ardhi na Mipango kuharakisha mchakato wa kidijitali katika sajili zote za ardhi nchini ili kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma na kusaidia kudhibiti udanganyifu wa masuala ya ardhi.

Korir alisisitiza dhamira ya idara hiyo ya kuendeleza uwazi, usimamizi bora wa fedha za umma na kuzingatia misingi ya utawala bora katika kutekeleza majukumu yake.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Mwenyekiti wa PAC, Amina Udgoon Siyad, ambaye alishiriki kwa njia ya mtandao, pamoja na wajumbe wengine wa kamati na maafisa wakuu kutoka Idara ya Ardhi na Mipango ya Kimaeneo.

Mjadala huo ulidhihirisha juhudi za idara hiyo za kuimarisha uwajibikaji, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.

Share This Article