Maafisa wakuu watatu wa benki washtakiwa kwa ufujaji wa fedha

Watatu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Agosti 11, 2026, baada ya mahakama kutoa ilani ya kuwataka kufika mbele yake.

Tom Mathinji
2 Min Read
Maafisa Wakuu watatu wa benki kushtakiwa kwa ufujaji wa pesa.

Maafisa wakuu watendaji wa benki za NCBA, KCB na Co-operative, wamefunguliwa mashtaka kwa madai ya kukosa kuripoti shilingi milioni 363.4  zinazodaiwa kupatikana kwa njia ya uhalifu.

Kulingana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), watatu hao wanalaumiwa kwa kukosa kuripoti mapatao yanayoshukiwa kuwa ya uhalifu kuambatana na sehemu ya 5 na ile ya 44(2) kuhusu mapato ya uhalifu na ulanguzi wa fedha ya sheria za Kenya.

Maafisa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Agosti 11, 2026, baada ya mahakama kutoa ilani ya kuwataka kufika mbele yake.

Wakati huo huo, ODPP pia imemshitaki mwakilishi wadi mteule kwa madai ya kuiba shilingi 363,420,459 kutoka kwa kampuni ya First Assurance Investment Company Limited, ambako alihudumu kama mkurugenzi pamoja na Gavana wa Lamu Issa Abdalla Issa.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Nora Otieno na Kiongozi Mkuu wa Mashtaka Willy Momanyi, waliiambia mahakama kwamba mwakilishi wadi huyo wa zamani aliiba fedha hizo kati ya Mei 18, 2018 na Aprili 30, 2024.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa mshukiwa huyo alitumia wadhifa wake kama Mkurugenzi kuingia kwenye akaunti za benki za kampuni hiyo zilizoko NCBA, KCB  na Co-operative kutoa fedha.

Kufuatia uchunguzi wa kina, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma amemfungulia mwakilishi wadi huyo mashtaka 120, yanayojumuisha kupanga ufujaji, mashtaka mawili ya wizi, mashtaka 114 ya kughushi stakabadhi na shtaka moja la kujipatia fedha za wizi.

Mwakilishi wadi huyo anadaiwa alighushi saini ya Mkurugenzi mwenza Gavana Issa Abdalla Issa kwenye hundi kadhaa za kampuni hiyo.

Share This Article