Obado na wengine warejea mahakamani kwa kesi ya ufisadi

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa zamani wa kaunti ya Migori Zachary Okoth Obado na washtakiwa wenza 15 leo wanafikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Milimani jijini Nairobi kwa ajili ya kesi ya ufisadi wa bilioni 1.98.

Obado na wenzake wanaojumuisha wanawe wanne wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi kwa wizi wa pesa za umma na ya mkinzano wa maslahi katika serikali ya kaunti ya Migori.

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, inasema kwamba mashahidi 59, watatoa ushahidi mahakamani katika hatua inayonuiwa kudhibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Wiki iliyopita EACC ilikanusha madai ya seneta wa kaunti ya Nairobi kwamba afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP ilikuwa imeondolea mbali kesi dhidi ya Obado na wenzake kutoa fursa ya kutatuliwa nje ya mahakama.

Akizungumza katika bunge la Seneti Jumatano wiki jana, Sifuna alisema kwamba aliduwazwa na ripoti kwamba ODPP ilikuwa imeweka ombi mahakamani la kuondoa kesi ya ufisadi dhidi ya Obado na wengine, na kwamba alikuwa amekubali kurejesha milioni 300.

Katika taarifa kwenye mtandao wa X, EACC ilielezea kwamba Obado na wenzake wanafikishwa mbele ya hakimu mkuu Victor Wakumile, ambapo shahidi wa kwanza ambaye ni mtafiti wa EACC atatoa maelezo ya jinsi washukiwa walibuni na kutekeleza mpango mzima wa ulaghai.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *