Kamati ya Olimpiki ya Kenya, NOC-K imezindua mpango wa mazoezi maalum kwa wanariadha wa mbio za masafa mafupi kujitayarisha kwa mashindano ya Olimpiki yatakayoandaliwa jijini Paris, Ufaransa mwaka huu.
Timu zitakazopelekwa nje ya nchi kwa mazoezi hayo ni zile za mbio za kupokezana kijiti za mita 100 kwa wanariadha wanne wanaume, mita 400 kwa wanariadha wanne wanaume, mita 400 kwa wakimbiaji wanne wanawake na timu ya mbio za kupokezana kijiti mseto.
Wanariadha hao walianza mazoezi katika uwanja wa taifa wa Nyayo siku ya Alhamisi chini ya kocha Mwaniki Mlamba.
Chini ya mpango huo, wanariadha hao watapokea mafunzo maalum pamoja na vifaa vya mazoezi.
Wanariadha hao 17 wametengewa shilingi milioni 5 na NOC-K ambazo zitagharimia kushiriki kwao kwa mashindano ya ASA Grand Prix continental tour challenge mjini Johannesburg, nchini Afrika Kusini kabla ya kuelekea kwa kambi ya mazoezi mjini Miramas na baadaye kushiriki mashindano ya Penny Relays na hatimaye mashindanoya dunia ya kupokezana kijiti nchini Bahamas kati ya Mei 4 na 5 mwaka huu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na kinara wa NOC-K Paul Tergat, Katibu Mkuu wa NOC-K Francis Mutuku na Mkurugenzi wa Riadha ya Chipukizi katika Chama cha Riadha Kenya, Barnabas Korir.