Viongozi wa kijeshi ambao wanaongoza nchi ya Niger, wamezindua bomba kubwa la kusafirisha mafuta ambayo hayajasafishwa hadi nchi jirani ya Benin, haya ni kwa mujibu wa kituo cha runinga cha kitaifa nchini humo.
Bomba hilo la urefu wa kilomita kama elfu 2, litawezesha Niger, moja ya nchi maskini zaidi ulimwenguni, kuuza mafuta hayo katika soko la kimataifa kwa mara ya kwanza kupitia bandari ya Seme nchini Benin.
Hafla ya kuzindua bomba hilo iliandaliwa katika eneo la Agadem lenye mafuta, kilomita kama 1700 kutoka jiji kuu Niamey, katika eneo la jangwa la Difa.
Waziri mkuu Ali Mahaman Lamine Zeine alisema kwamba mapato yatakayotokana na mafuta hayo, yatatumika kuhakikisha uhuru na maendeleo ya nchi yao.
Mpaka kati ya Niger na Benin umefungwa kufuatia vikwazo vikali vilivyowekwa na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, dhidi ya Niger kufuatia mapinduzi ya Julai 26.
Mawaziri wa kawi wa nchi za Mali na Burkina Faso, ambao wameunga mkono viongozi wapya wa Niger na ambao pia wameshuhudia mapinduzi ya kijeshi katika muda wa miaka miwili iliyopita, walihudhuria hafla hiyo.
Mradi huo wa bomba ulikuwa unafaa kukamilika mwaka 2022 lakini ukakwamishwa na janga la Covid-19
kulingana na mwanakandarasi.
Kampuni ya China National Petroleum Corporation (CNPC) ndiyo inachimba mafuta hayo.
Dola bilioni 6 zimewekezwa kwenye mradi huo kulingana na serikali ya Niger, zikiwemo bilioni 4 za kuboresha maeneo ya kuchimba mafuta na bilioni 2.3 za kuunda bomba hilo.
Uwekezaji huo umeongeza uzalishaji mafuta nchini Niger hadi mapipa 110,000 kwa siku, huku lengo likiwa mapipa 200,000 kufikia mwaka 2026.
Niger ilikuwa imeghubikwa na maandamano ya kila mara ya kutaka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini humo kabla ya mapinduzi yaliyombandua mamlakani rais Mohamed Bazoum.
Nchi nyingi za magharibi zimekatiza misaada ya maendeleo kwa Niger huku benki ya dunia ikionya kwamba pato jumla la taifa hilo huenda likapungua kwa asilimia 2.3 mwaka huu iwapo vikwazo vya kimataifa vitaendelea.