Mwanamuziki wa Kenya Nazizi Hirji alionekana kuzidiwa na hisia wakati yeye na familia yake walikuwa wakipiga picha za pamoja.
Nazizi, mume wake na mwanao walikuwa wamevaa mavazi yaliyofanana wakati wa shughuli hiyo, huku wakiwa wameshika picha ya mwanawe ambaye alifariki. Nazizi hakuweza kuficha hisia zake kila alipoangalia picha ya mtoto Jazeel.
Video fupi ya shughuli hiyo ya upigaji picha ilichapishwa na kampuni moja ya mavazi ambayo ilikiri kwamba ilikuwa shughuli ngumu zaidi kwao.
“Wakati Nazizi aliwasiliana nasi na kuomba kwamba tumuenzi na kumkumbuka mwanawe Jazeel Adam, tulihisi tumeheshimiwa pakubwa.” taarifa ya kampuni hiyo ilisema.
Kampuni hiyo ilisema kwamba familia ya Nazizi imekuwa yenye ukarimu kwa nembo yao na wakawashukuru kwa uwazi wao.
Wahudumu wa kampuni hiyo wanamkumbuka mtoto Jazeel kama ambaye alipenda watu, alikuwa mwenye nguvu na aliweza kuitikia kazi ya kuonyesha mavazi yao vyema.
Jazeel alifariki siku ya Krismasi mwaka 2023 nchini Tanzania kwenye hoteli moja ambako familia yake ilikuwa imekwenda kwa ajili ya likizo.
Anaripotiwa kufa maji baada ya kuanguka kwenye kidimbwi cha kuogelea cha hoteli hiyo.