Mamlaka ya kudhibiti usafiri wa ardhini nchini Tanzania yaani Land Transport Regulatory Authority – LaTRA imetangaza nauli mpya zitakazotozwa na magari ya kusafirisha abiria nchini humo almaarufu daladala.
Mkurugenzi mkuu wa LaTRA Habibu Suluo alitangaza hayo katika kikao na wanahabari mjini Arusha ambapo alifafanua kwamba nauli ya chini ni shilingi 600 za Tanzania sawa na shilingi 37 za Kenya huku kiwango cha juu zaidi kikiwa shilingi 1400 za Tanzania sawa na shilingi 86 za Kenya.
Suluo alisema kwamba waliafikia hatua ya kupandisha nauli baada ya kuzingatia mambo mengi na wala sio bei ya mafuta tu.
Alisema sababu zilizochangia ongezeko la nauli ni pamoja na gharama ya uwekezaji, gharama ya uendeshaji biashara, gharama ya kutengeneza magari, gharama ya kupungua kwa thamani ya magari, ada wanazotozwa wamiliki wa magari na mengine.
Idadi ya abiria ambao gari inaweza kubeba kwa wakati mmoja na uwezo wa kuzijaza abiria pia vilizingatiwa kwa kuafikia nauli mpya na hata mizunguko ambayo gari linafanya kwa kila siku.
Suluo alisema walipiga hesabu zao vizuri na nauli hizo hazitaathiriwa na lolote ili ziongezeke tena ghafla ila huenda hilo likafanyika baada ya mwaka mmoja.