Naibu Rais Rigathi Gachagua asema yaliyoshuhudiwa jana ni aibu

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametaja maandamano yaliyoshuhudiwa jana katika sehemu mbali mbali za nchi kuwa aibu.

Akizungumza leo jijini Nairobi wakati wa kufungua mkutano wa wabunge kuhusu utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, Gachagua alijutia vifo na uharibifu wa mali katika sehemu mbali mbali za nchi wakati wa maandamano.

“Sitaki kusema sana kuhusu yaliyotendeka, ni ya aibu na hayastahili maoni yangu.” alisema Gachagua.

Naibu Rais badala yake alihimiza viongozi waliochaguliwa wazingatie kazi yao kwani wana mkataba na waliowachagua na hawaendi popote hadi muda wao wa miaka mitano ukamilike.

Alitoa mfano wake na Rais William Ruto akisema wana mkataba wa miaka mitano na wakenya ambao unaweza kuongezwa au kukatizwa sawa na mikataba yao na wananchi wa kenya.

Maandamano ya jana yalisababisha uharibifu katika sehemu mbali mbali nchini kama vile barabara ya Expressway iliyoharibiwa katika kituo cha Syokimau. Waandamanaji walinakiliwa kwenye video wakiharibu vizuizi vya barabara hiyo na kusababisha kampuni inayosimamia barabara hiyo kufunga kituo hicho.

Waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen anazuru barabara hiyo leo kutathmini uharibifu uliotekelezwa. Alisema kwenye taarifa jana kwamba wameomba afisi ya upelelezi wa jinai ichunguze na kukamata wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Ripoti zinaashiria kwamba mvulana mmoja wa miaka 18 alipigwa risasi na maafisa wa polisi mjini Emali katika kaunti ya Makueni wakati wa maandamano ya jana.

Gavana wa kaunti ya Makueni Mutula Kilonzo Junior alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo akielezea kwamba mvulana huyo kwa jina Brian Muendo ambaye alikuwa anasubiri kujiunga na chuo kikuu cha Kenyatta hakuwa anahusika na maandamano bali alikuwa ametoka tu nje kuona yaliyokuwa yakijiri.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *