Mwenyekiti wa IEBC ataka gharama za uchaguzi kupunguzwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Eratus Ethekon ametoa wito wa kupunguzwa kwa gharama za uchaguzi nchini ambazo zimekuwa zikigharimu mabilioni ya pesa miaka nenda miaka rudi.

Anasema hilo linaweza tu kufikiwa ikiwa kutakuwa na uadilifu katika mchakato wa utayarishaji bajeti.

“Tunapofanyia kazi takwimu hizi, hazipaswi kuwa tu zisizokuwa na mantiki. Kila pendekezo linapaswa kuwa halisi, lenye msingi, na linalowiana na malengo yetu ya kitaasisi,” alisema Ethekon wakati wa kongamano la IEBC la kutayarisha Mpangokazi wa Matumizi ya Kipindi cha Kati (MTEF) wa mwaka 2026/27, 2027/28  na 2028/29.

“Bajeti tunayotayarisha hapa haihusu tu takwimu bali ni mwongozo wa kujenga imani na uaminifu katika mchakato wetu wa uchaguzi.”

Ethekon akisisitiza umuhimu wa uadilifu katika utayarishaji bajeti ili kuisaidia nchi kupunguza gharama za uchaguzi kwa kutumia ipasavyo rasilimali chache zilizopo bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa.

Matamshi sawia yalitolewa na Naibu Mwenyekiti wa IEBC Fahima Araphat Abdallah ambaye anaongoza kamati ya fedha na ununuzi ya tume hiyo.

Abdallah alisisitiza kuwa kongamano hilo ni msingi wa mipango ya fedha na matayarisho ya uchaguzi kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Aliongeza kuwa kuna haja ya kuunda bajeti inayozingatia waraka wa Wizara ya Fedha, kuunga mkono shughuli za IEBC na kuakisi ukweli wa kiuchumi wakati pia ikidumisha mamlaka ya kikatiba ya tume hiyo.

 

 

Website |  + posts
Share This Article