Mradi wa kitaifa wa nyumba za gharama nafuu uliangaziwa kwa njia ya kipekee kwenye sherehe za mwaka huu za Madaraka katika kaunti ya Homa Bay.
Hata ingawa kauli mbiu ilikuwa Uchumi Samawati na Shughuli za Baharini, itifaki ilivunjwa pale ambapo mfawidhi alisimamisha kwa muda makaribisho ya Naibu Rais Kithure Kindiki kutoa nafasi kwa katibu wa wizara ya nyumba Charles Hinga.
Hinga katika taarifa yake kuhusu mradi wa nyumba za gharama nafuu alisema kwamba tunaelekea kunakofaa akisema kwamba orodha ya wakenya wanaokuwa wamiliki wa nyumba inaendelea kuongezeka kutokana na mradi huo.
Alialika wakenya watatu Damaris Adoyo Ochele, Victor Okoyo ambaye ni mlemavu na Hellen Osala ambao Rais aliwapa vyeti rasmi vya umiliki wa nyumba hizo za gharama nafuu.
Na katika hotuba yake, Rais William Ruto alitaja mradi huo unaoendelea katika sehemu mbali mbali za Kenya, kuwa nembo muhimu ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
“Wiki iliyopita, nilijaliwa fursa ya kutoa funguo za nyumba za kwanza 1,080 za mradi huu katika mtaa mpya wa Mukuru huko Nairobi” alisema Rais Ruto akiongeza kusema kwamba ulikuwa wakati mzuri na wa mabadiliko kwa maisha ya walionufaika.
Alisema hafla hiyo iliashiria pia hatua muhimu kwa Kenya na ilionyesha kwamba miradi ya kitaifa inaweza kutekelezwa kikamilifu, kunufaisha wananchi wa kawaida na kubadili uelewa wa mabadiliko ya maana.
“Yapata miaka miwili iliyopita wengi walishuku wakati tulisema wakenya wa kawaida wataanza kumiliki nyumba kupitia mpango wa kukodisha na baadaye kumiliki wakitumia kiasi kile kile cha pesa ambazo wangelipia kodi ya nyumba” alisema Rais akiongeza kwamba ahadi hiyo sasa imeanza kutekelezwa.