Rais William Ruto leo aliwapunga waliohudhuria sherehe za mwaka huu za Madaraka katika uwanja wa Raila Odinga kaunti ya Homa Bay pale ambapo alitamka maneno ya lugha ya dholuo ya wimbo wa msanii maarufu Prince Indah.
Alikuwa akikamilisha hotuba yake ya siku ya leo ambapo alisema, “Ndio mwimbaji mmoja hapa akatuambia Wan waonge wasi wasi, wan waonge wach, wan wachuodho mana tich”.
Kiongozi wa nchi alirudia maneno hayo huku akishangiliwa na umma na kutoa maana ya maneno hayo akiwatania Naibu Rais Kithure Kindiki na Raila Odinga ambao alisema huenda wasielewe lugha ya dholuo.
Alisema maneno hayo yanatafsiriwa kwa Kiswahili kama “Hatuna wasi wasi, Hatuna midomo mingi, Tunachapa kazi” na kumalizia kwamba “Ile kazi bila break ndiyo tunachapa.”
Prince Indah ametumia fursa ya maneno ya wimbo wake uitwao “Osiepe” kutumiwa na Rais Ruto kutangaza tamasha lake la usiku wa leo katika hoteli moja mjini Homa Bay.
Katika akaunti yake ya Instagram, msanii huyo amechapisha picha inayomwonyesha akiwa jukwaani akaandika maneno aliyoyasema Rais na kutangaza pia wimbo wake na Jose Chameleone utakaotolewa rasmi Juni 9, 2025.