Rais William Ruto amepokea hati za utambulisho za mabalozi sita wapya leo katika ikulu ya Nairobi ambao ni Ernest Rwamucyo wa Rwanda, Anthony Louis Kon wa Sudan Kusini, Peter Kakowou Lavahun wa Sierra Leone, Chiranjib Sarker wa Bangladesh, Erika Álvarez Rodríguez wa Jamhuri ya Dominica na Kan Yaw Kiong wa Singapore.
Balozi Ernest Rwamucyo amepandishwa cheo na kufanywa balozi wa Rwanda nchini Kenya, jukumu atakalotekeleza kwa wakati mmoja katika nchi za Somalia na Eritrea.
Anawakilisha Rwanda pia katika shirika la umoja wa mataifa kuhusu mazingira na lile la makazi katika wadhifa wa kudumu.
Balozi mpya wa Sudan Kusini nchini Kenya Kon amekuwa mwanadiplomasia kwa muda mrefu akihudumia Sudan na Sudan Kusini. Kabla Sudan Kusini ipate uhuru, alikuwa akihudumu kama balozi wa Sudan nchini DRC na Congo, Brazzaville.
Luteni Jenerali Peter Kakowou Lavahun atakuwa mwakilishi wa tatu wa Sierra Leone nchini Kenya na anachukua pia wadhifa wa mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika afisi za Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, shirika la UNEP na UN-Habitat.
Kabla ya kuingilia uanadiplomasia, Lavahun alihudumu katika sekta ya usalama ambako alipanda cheo hadi akawa mkuu wa jeshi la Sierra Leone.
Balozi Sarker wa Bangladesh amekuwa akihudumu kama naibu balozi nchini India kabla ya kupandishwa cheo na kutumwa nchini Kenya.
Erika Álvarez Rodríguez wa Jamhuri ya Dominica amekuwa mwanadiplomasia kwa miaka 27 sasa ambapo amehudumu katika wizara ya masuala ya kigeni ya nchi yake.
Balozi mpya wa Singapore Kiong amekuwa kihudumu katika nyadhifa mbali mbali za sekta ya kibinafsi katika nchi yake na huko Ulaya kabla ya kuteuliwa kuwa balozi.
Rais Ruto alikubali hati za mabalozi hao za utambulisho huku akiwashauri waangazie maslahi ya mataifa yao nchini Kenya na kukuza uhusiano mwema kati ya Kenya na mataifa yao.