Mwanamume akamatwa Thika kisa mzozo wa kimapenzi

Aliingia kwa nguvu kwa nyumba na kuharibu mali kufuatia mzozo na mwanamke aliyekutana naye kwenye mitandao ya kijamii.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamume mmoja mkazi wa Thika anayefanya kazi ya uashi amekamatwa na kuwekwa kizuizini na polisi kisa mzozo wa kimapenzi uliomfanya aharibu mali.

Anatuhumiwa kuingia kwa nguvu kwenye nyumba moja ya makazi na kuharibu mali kufuatia mzozo uliohusishwa na mwanamke aliyekuwa amekutana naye kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, Fred alikuwa akiwasiliana na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Tash kwa wiki tatu kabla ya kupanga kukutana naye ana kwa ana kwa mara ya kwanza.

Fred anaripotiwa kuandaa chakula maalumu na kumtumia Tash Shilingi 1,500 za nauli alizoomba, na kumwongezea pesa zaidi baada ya mwanamke huyo kudai kuwa bado alikuwa amekwama njiani.

Hata hivyo, licha ya kutoa ahadi mara kadhaa kwamba alikuwa njiani, Tash hakufika na akatoweka kwenye WhatsApp.

Akiwa amekasirika, Fred anaripotiwa kuelekea Makongeni, alikoamini mwanamke huyo anaishi, na kujaribu kuingia katika nyumba yake. Mlinzi alimzuia, lakini akaingia kwa nguvu ndani ya jengo hilo na kuharibu mlango wa nyumba.

Alishtuka kugundua kuwa Tash alikuwa mke wa mtu, hali iliyosababisha makabiliano kati yake, mume wa Tash na majirani.

Vurugu zilipotokea, Fred anadaiwa kuharibu gari alipokuwa akijaribu kutoroka kabla ya kukamatwa na maafisa wa DCI.

Kwa sasa, anazuiliwa na polisi huku akikabiliwa na malalamishi yanayohusiana na kusababisha vurugu na kuharibu mali.

Wakenya wameshauriwa kuwa waangalifu wanapokutana na watu wasiowafahamu mitandaoni, kuepuka kutuma pesa kwa watu wasiowajua vizuri na kutatua migogoro kihalali.

Share This Article