Mr. Sugu asema hatanyoa mpaka Lissu awe huru!

Awali alikuwa ameonyesha matumaini kwamba Lissu angeachiwa huru Ijumaa na kwamba wangenyoa nywele.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki na mwanasiasa wa Tanzania Mr. Sugu au Joseph Mbilinyi, amesema kwamba ataendelea kufuga nywele hadi pale ambapo mwenyekiti wa chama chake CHADEMA Tundu Lissu atakuwa huru.

Siku moja kabla ya hukumu ya Lissu kusomwa, Mbilinyi alikuwa ameandika ujumbe wa matumaini kwenye mitandao ya kijamii, akiamini kwamba Lissu angeachiwa huru.

“Natumai kesho TUNANYOA na maisha mengine yaendeleee… Mwenyekiti wetu Lissu ameshikilia amani ,furaha na utulivu kwa hivyo akiwa huru kesho hakika nchi itaanza kupona!” aliandika Mbilinyi.

Alimalizia ujumbe huo na ombi kwa Mungu awasimamie na awape nguvu na ujasiri wa kusimamia haki majaji husika.

Lakini Ijumaa ilipojiri Lissu akaondolewa mashtaka ya uhaini na kufungwa miaka minne gerezani kwa madai ya uchochezi, Mbilinyi alikatizwa tamaa.

Keshoye aliandika, “Jana ilikuwa BLACK FRIDAY… Another DARK CHAPTER kwa nchi yetu…” kuonyesha kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa.

Jana jumapili msanii huyo aliandika, “Kuna watu wananiuliza eti kwa vile Mwenyekiti wetu ameshafungwa (kihuni) eti sasa NITANYOA?”

Aliambia mashabiki zake kwamba kamwe hatonyoa wala kuchana nywele mpaka Lissu atoke jela.

Wanachama wa CHADEMA wamekuwa wakisusia kunyoa nywele tangu alipozuiliwa Lissu Aprili 2025 kama njia ya kusimama naye anapotafuta haki.

Familia ya Tundu Lissu nayo ilikuwa imesimamisha mazishi ya kakake kusubiri hukumu yake.

Share This Article