Familia ya mwanamke aliyepatikana ameuawa Kasarani yatoa taarifa

Marion Bosire
1 Min Read

Familia ya mwanamke aliyepatikana ameuawa na mwili wake kuwekwa kwenye karatasi huko Roysambu Kasarani hatimaye imejitokeza.

Kulingana na familia, msichana huyo anaitwa Rita Waeni Muendo wa umri wa miaka 20 na alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha JKUAT ambako alikuwa aanze mwaka wake wa nne wa masomo.

Mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa bila kichwa ambacho kinatafutwa hadi sasa.

Jamaa zake wanaelezea kwamba alitoka nyumbani kwa shangazi yake eneo la Syokimau katika kaunti ya Machakos Jumamosi, Januari 13, 2024 akienda kukutana na rafiki yake mjini Nairobi na hakurejea tena.

Baba ya msichana huyo alipokea ujumbe kutoka kwa simu ya Waeni wa kuitisha fidia ya shilingi laki 5, Jumapili, Januari 14, 2024 saa 11 alfajiri.

Jumbe nyingine mbili zilitumwa za kuitisha kiwango hicho cha fidia katika muda wa saa 24 lakini hakukuwa na maelezo kuhusu namna ya kuiwasilisha.

Sasa imebainika kwamba jumbe hizo zilitumwa hata baada ya Waeni kuuawa ikilinganishwa na wakati taarifa ya kifo chake ilijulikana.

Familia hiyo sasa imeomba umma kuipatia muda wa kumwomboleza mwanao huku ikishukuru maafisa wa DCI kwa kuendeleza uchunguzi.

Mshukiwa mmoja ambaye anachunguzwa alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ili kubaini iwapo ndiye mhusika wa mauaji ya Waeni.

Share This Article