Mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani Silentó amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kutokana na hatia ya kumuua binamu yake mwaka 2021.
Silentó wa umri wa miaka 27 kutoka Atlanta, Georgia nchini Marekani ambaye jina lake halisi ni Ricky Lamar Hawk, alikubali mashtaka ya kuua bila kukusudia na mashtaka mengine yaliyotokana na kisa cha mauaji ya binamu yake wa umri wa miaka 34.
Alikubali pia mashtaka ya kumdhulumu mwendazake, kuwa na bunduki akitekeleza uhalifu na kuficha habari kuhusu kifo cha mwenzake. Aliondolewa mashtaka ya mauaji kama sehemu ya makubaliano ya kukiri makosa yake.
Maafisa wa polisi wa jimbo la DeKalb walipata mwili wa Frederick Rooks III binamu ya Silentó ukiwa na majeraha ya risasi huku maganda 10 ya risasi yakipatikana karibu naye asubuhi ya Januari 21, 2021.
Video iliyonakiliwa na kamera za ulinzi ilionyesha gari ya rangi nyeupe aina ya BMW ikiondoka eneo la tukio dakika chache baada ya ufyatuaji risasi.
Polisi walithibitisha kwamba gari hiyo ndiyo Hawk alitumia kumchukua Rooks.Hawk alikamatwa Februari Mosi, 2021 na kukiri kumpiga risasi Rooks.
Jamaa za Rooks walitaka Silento ahukumiwe kifungo cha muda mrefu gerezani.