Mwanamuziki Willy Paul amefurahikia mustakabali wake katika tasnia ya muziki baada ya kukutana na mhusika mkuu wa tuzo kubwa zaidi za muziki duniani za Grammy.
Paul ambaye alikuwa amejawa na furaha alichapisha video fupi inayomwonyesha akijadiliana na Panos A. Panay ambaye ni Rais wa taasisi andalizi ya tuzo za Grammy.
Aliandika, “Unajua nini! Nimekutana na Rais wa tuzo za Grammy Panos A. Panay, amesikiliza wimbo wangu mpya ambao nimehusisha msanii Guchi wa Nigeria na ameupenda”.
Msanii huyo aliendelea kwa kuhakikishia mashabiki wake kwamba mustakabali wake ni mzuri huku akishukuru wote ambao wamemuunga mkono katika safari yake kama mwanamuziki.
“Kwa wote ambao mmeniunga mkono hadi sasa asante. Naingia huko juu sai sai! Grammy inakuja” alimalizia msanii huyo wa Kenya.
Willy ambaye jina lake halisi ni Wilson Abubakar Radido ni mwanamuziki wa Kenya wa umri wa miaka 31 sasa na aliingilia muziki mwaka 2010.
Alianzia katika sekta ya nyimbo za injili akiwa na mwenzake Bahati kabla yao kugura na kuingilia muziki wa dunia.